Friday, November 7, 2014

TIKETI ZA ELEKTRONIKI KUTOUZWA KWENYE MAGARI.

LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea wikiendi hii ambapo tiketi za elektroniki hazitauzwa tena kwenye magari, hivyo washabiki wanunue tiketi hizo kwenye mtandao au kwenye maduka ya CRDB Fahari Huduma. Kesho (Novemba 8 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutakuwa na mechi kati ya Yanga na Mgambo Shooting wakati Uwanja wa Chamazi kutakuwa na mechi kati ya Azam na Coastal Union. Jumapili ni mechi kati ya Simba na Ruvu Shooting. Viingilio kwenye mechi za Uwanja wa Taifa ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu, sh. 8,000 (viti vya rangi ya chungwa), sh. 15,000 (VIP B na C) wakati VIP A itakuwa sh. 20,000. Mechi za Uwanja wa Chamazi kiingilio ni sh. 3,000 kwa sh. 10,000. Mechi nyingine za VPL kesho ni kati ya Stand United na Mbeya City (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga), Mtibwa Sugar na Kagera Sugar (Uwanja wa Manungu, Morogoro). Raundi hiyo ya saba itakamilika Jumapili kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam kwa mechi kati ya JKT Ruvu na Ndanda kutoka Mtwara. Wakati huo huo, mchezaji bora wa VPL kwa mwezi Oktoba, Salum Abubakar wa Azam atakabidhiwa zawadi yake kesho (Novemba 8 mwaka huu) kabla ya mechi kati ya Azam na Coastal Union.

No comments:

Post a Comment