Wednesday, November 5, 2014

UEFA CHAMPIONS LEAGUE 2014: MADRID, DORTMUND ZAWA TIMU ZA KWANZA KUFUZU HATUA YA 16 BORA.

MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi iliendelea tena jana huku tukishuhudia klabu mbili za Borussia Dortmund na Real Madrid zikifanikiwa kutinga hatua inayofuata ya timu 16 bora. Dortmund wanaonolewa na Jurgen Klopp pamoja na kusuasua katika Bundesliga lakini katika michuano hiyo wamekuwa wakionyesha kiwango kizuri baada ya kuigaragaza Galatasaray kwa mabao 4-1 hivyo kuwa wameshinda mechi zao zote nne katika kundi D. Madrid wao walitinga hatua hiyo baada ya kuikabili Liverpool na kuitandika bao 1-0 katika Uwanja wa Santiago Bernabeu na kufikisha alama 12 katika kundi B mbele ya FC Basel waliopo nafasi ya pili ambao nao waliichapa Ludogorets Razgrad kwa mabao 4-0. Kwa upande mwingine ushindi wa mabao 2-0 waliopata Atletico Madrid dhidi ya Malmo umewapaisha mpaka kileleni mwa kundi A huku Olympiakos wakiwa nafasi ya pili pamoja na kutandikwa na Juventus kwa mabao 3-2. Kundi C Bayer Leverkusen wamejiimarisha kileleni baada ya kuibuka na ushindi wa ugenini wa mabao 2-1 dhidi ya Zenit Saint Petersburg, Benfica wao walifufua matumaini yao ya kusonga mbele baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Monaco. Arsenal wao wameendelea kushika nafasi ya pili nyuma ya Dortmund baada ya kushindwa kulinda ushindi wake na kujikuta wakitoa sare ya mabao 3-3 na Anderletch katika Uwanja wa Emirates.

No comments:

Post a Comment