MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya imeendelea tena jana na kushuhudia timu za Barcelona, Bayern Munich, Paris Saint-Germain-PSG na FC Porto nazo zikifuzu hatua ya timu 16 bora baada ya kushinda michezo yao. Katika michezo ya michuano hiyo iliyochezwa juzi mabingwa watetezi Real Madrid na Borussia Dortmund nao walitangulia katika hatua hiyo baada ya kushinda mechi zao. Barcelona wao walifanikiwa kusonga mbele baada ya kuitandika Ajax Amsterdam kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na nyota wake Lionel Messi wakati Bayern Munich wao waliichapa kwa mara nyingine AS Roma kwa mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika Allianz Arena. PSG wao walisonga mbele baada ya kuitandika Apoel kwa bao 1-0 huku Porto nao wakicharuka na kuichapa Athletic Bilbao kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na nyota wa Colombia Jackson Martinez na Mualgeria Yacine Brahimi. Wiki hii imekuwa mbaya kwa timu za Uingereza kwani baada ya Liverpool kuiweka rehani nafasi yao ya kusonga mbele kwa kufungwa na Madrid kwa bao 1-0 huku Arsenal waking’ang’aniwa sare nyumbani na Anderlecht, Chelsea nao wameingia katika mkumbo huo baada ya kugawana alama na Maribor kwa kutoka sare ya bao 1-1. Kwa upande wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu hali yao ndio imezidi kuwa mbaya baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya CSKA Moscow ya Urusi katika Uwanja wa Etihad na kuweka matumaini yao ya kusonga mbele katika mashaka.
No comments:
Post a Comment