SHIRIKISHO la Kimataifa la Mashindano ya Langalanga limechapisha ripoti yake kuhusiana na ajali katika mashindano ya Grand Prix ya Japan ambayo yalimuacha Jules Bianchi na majeraha ya kichwa. Katika ripoti hiyo shirikisho hilo limehakikisha halitoi lawama kwa yeyote huku wakiweka mikakati madhubuti kuhakikisha tukio kama hilo halitokei siku za usoni. Moja ya mambo yaliyotajwa katika ripoti hiyo ni dereva Jules Bianchi kutopunguza mwendo inavyostahili pindi alipoonyeshwa bendera mbili za njano ambazo zilikuwa zikiashiria hatari iliyoko mbele. Hata hivyo jambo hilo sio geni kwa madereva wa langalanga pindi wanapokuwa katika mashindano hayo kwani wengi wao wamekuwa wakichukua tahadhari kidogo pindi waonyeshwapo alama hizo. Kutoka na hilo msimu ujao kitafungwa kifaa maalumu katika magari hayo ambapo kama kutatokea ishara kama hiyo gari lenyewe litajipunguza mwendo mpaka kufikia ule ambao inaweza kusimama kama kuna kitu cha ghafla mbele.

No comments:
Post a Comment