Monday, December 22, 2014

MASHABIKI WA SOKA KUANZA KURUHUSIWA TENA KUTIZAMA MECHI ZA LIGI MISRI.

MASHABIKI wa soka wa Misri wanatarajiwa kuruhusiwa kuhudhuria mechi za Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka mitatu. Mashabiki nchini humo walikuwa wamefungiwa kuhudhuria mechi za ligi ya nyumbani toka tukio la Port Said Februari mwaka 2012 wakati zilipozuka vurugu ambazo zilipelekea vifo vya zaidi ya watu 70. Chama cha Soka nchini humo-EFA kimedai kuwa wizara ya mambo ya nchi na wizara ya michezo na vijana wamekubaliana kuruhusu mashabiki kuhudhuria mechi za Ligi Kuu wakati itakapoanza mzunguko wake wa pili. EFA imefafanua kuwa mashabiki wapatao 10,000 wataruhusiwa katika mechi zitakazochezwa katika viwanja vilivyopo Cairo na Alexandria huku wengine 5,000 wakiruhusiwa katika viwanja vidogo nchini humo. Hata hivyo adhabu itaendelea kwa michezo itakayohusisha vilabu vyovyote kati ya sita vikubwa nchini humo. Klabu za Al Ahly, Zamalek, Al Ittihad, Ismaily, Al Masry na Damanhur zote zitaendelea kucheza katika uwanja mtupu pindi mojawapo itakapokutana na mwenzake.

No comments:

Post a Comment