Tuesday, December 9, 2014

MOURINHO KUMPANGA COSTA KATIKA MCHEZO DHIDI YA SPORTING LISBON.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho bado anafikiria kumpanga Diego Costa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kesho dhidi ya Sporting Lisbon ili aweze kumuimarisha mshambuliaji huyo aliyekuwa majeruhi. Chelsea tayari imeshafuzu hatua ya mtoano ya michuano hiyo wakiwa vinara katika kundi lao pamoja na matokeo yeyote watakayopata katika mchezo wao huo wa mwisho wa kundi G utakaofanyika katika Uwanja wa Stamford Bridge. Kutokana na ratiba ngumu katika kipindi cha krismasi, itakuwa sio jambo la kushangaza kama Mourinho atawapumzisha nyota wake kadhaa wakiwemo Cesc Fabregas, Eden hazard na Thibaut Courtois wakati watakapocheza na Sporting hapo kesho. Lakini Costa anaweza asipumzishwe kwasababu Mourinho bado ana wasiwasi na afya ya mshambuliaji wake huyo ambaye amekuwa akiandamwa na majeruhi katika siku za karibuni. Toka Costa asajiliwe na Chelsea akitokea Atletico Madrid amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Mourinho kwa kufunga mabao saba katika mechi nne alizoitumikia timu hiyo lakini majeruhi yamekuwa kikwazo kikubwa kwa nyota huyo.

No comments:

Post a Comment