SHIRIKISHO la Soka la Burkina Faso bado linaendelea kumtilia ngumu kiungo Prejuce Nakoulma kutokana na kosa lake la kudanganya. Winga huyo mwenye umri wa miaka 27 alifungiwa na shirikisho hilo kwa kutosema ukweli kuhusiana na hali ya afya yake. Nakoulma ambaye anacheza katika klabu ya Mersin inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uturuki, aliomba kuachwa katika mechi za mwisho za kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika Novemba mwaka huu kutokana na sababu za kiafya. Nyota huyo ambaye alifunga bao katika fainali za mwaka jana za michuano hiyo alidai kupata majeruhi katika klabu yake lakini hakuwakilisha vielelezo katika benchi la ufundi wala shirikisho hilo ili kuthibitisha hali yake. Kutokana na hilo rais wa FBF alimsimamisha mchezaji huyo huku akionya kuwa wachezaji wanapaswa kuheshimu timu ya taifa na kudai kuwa hawatamuita mpaka hapo atakapoomba radhi au kuwakilisha vielelezo vinavyohitajika. Burkina Faso wamepangwa katika kundi A katika michuano hiyo ya mwakani wakiwa sambamba na wenyeji Guinea ya Ikweta, Congo Brazzaville na Gabon.
No comments:
Post a Comment