SHIRIKISHO la Soka nchini-TFF limetangaza kuwa klabu mahasimu nchini Simba na Yanga zitacheza katika mchezo maalumu wa Nani Mtani Jembe utakaofanyika Desemba 13 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Akizungumza na wanahabari Mkurugenzi wa Michezo wa TFF, Boniface Wambura amesema kiingilio katika mchezo huo kitaanzia shilingi 7,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu mzunguko. Kwa upande wa jukwaa maalumu au VIP C pamoja na viti vya rangi ya chungwa mzunguko kiingilio kitakuwa shilingi 15,000 huku VIP B kiingilio kikiwa shilingi 30,000. Wambura aliendela kudai kuwa mshindi katika mechi hiyo atajinyakulia kitita cha shilingi milioni 15 huku timu itakayofungwa ikiambulia shilingi milioni tano. Wambura amesema mchezo huo utakaoanza saa kumi kamili jioni utapigwa kwa dakika tisini pekee na kama mshindi hakupatikana timu zitakwenda moja kwa moja katika changamoto ya mikwaju ya penati hivyo kuwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kushangilia timu zao.
No comments:
Post a Comment