Tuesday, January 27, 2015

AFCON 2015: WASIWASI WATANDA KUHUSIANA NA HALI YA USALAMA BAADA YA WENYEJI KUPENYA ROBO FAINALI.

KUFUZU kwa wenyeji Guinea ya Ikweta katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika kumetengeneza wasiwasi juu ya usalama kwa waandaaji wa michuano hiyo. Wenyeji waliwashangaza majirani zao Gabon kwa kuwachapa mabao 2-0 Jumapili iliyopita na kumaliza katika nafasi ya pili katika kundi A. Guinea ya Ikweta sasa itachuana na Tunisia katika hatua ya robo fainali Jumamosi hii huko Ebibeyin. Lakini kuna wasiwasi kuwa uwanja huo mpya wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 5,000 pekee utakuwa mdogo kwa ajili ya mashabiki wengi wanaotegemewa katika mchezo huo. Michuano hiyo tayari imeshashuhudia mashabiki wakibomoa na kupita katika uzio katika mchezo wa ufunguzi uliofanyika Bata Januari 17 ambapo uwanja wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 35,000 ulifurika. Katika viwanja vingine mara kadhaa maeneo ya maalumu na sehemu za wanahabari zimekuwa zikivamiwa mara kadhaa na mashabiki huku polisi wakipambana kurejesha hali ya utulivu. Waandaaji sasa inabidi waangalie uwezekano wa kuupeleka mchezo huo katika Uwanja wa Bata ambao ndio mkubwa katika nchi hiyo ambapo tayari Guinea ya Ikweta wameshacheza mechi zao tatu huku mashabiki wakiwa wamejaa. Uwanja huo pia ndio utakaotumiwa kwa ajili ya mchezo wa fainali Februari 8.

No comments:

Post a Comment