PAMOJA na malalamiko ya hapa na pale michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika-Afcon imeanza kutimua vumbi leo kwa mchezo wa ufunguzi ambao unaoendelea hivi sasa ambao umewakutanisha wenyeji wa michuano hiyo Guinea na Ikweta na Burkina Faso huko Bata. Wiki nzima iliyopita kumekuwa na malalamiko kadha wakati timu zikiwasili nchini humo kwa ajili ya michuano hiyo kikubwa likiwa uhaba wa malazi, viwanja vibovu vya mazoezi pamoja na hofu juu nyasi za kuchezea ambazo bado ni mpya. Guinea ya Ikweta ilipata nafasi ya kuandaa michuano hiyo wakiwa na miezi miwili ya maandalizi baada ya mwenyeji wa awali Morocco kujitoa kutokana na hofu ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Afrika-CAF, Hicham el Amrani amesema michuano ya mwaka huu haitakuwa ya kupendeza kama ilivyozoeleka kwani kwa kawaida mwenyeji hupewa miaka minne ya kujiandaa lakini safari kulikuwa na siku zisizozidi 50. El Amrani aliendelea kudai kuwa Guinea ya Ikweta ni nchi ndogo huku sehemu kubwa ya wananchi wake wakiishi katika umasikini wa kupindukia hivyo matatizo kama suala la malazi na mengineyo yaliyotajwa yatakuwa changamoto katika michuano hiyo. Timu mbili tayari zimeshabadilisha hoteli mara baada ya kutua jijini Bata ambazo ni Congo Brazzaville na Burkina Faso kutokana na uchache wa vyumba vya kulala. Hata hivyo Amrani amedai pamoja na changamoto zote hizo zilizopo anadhani michuano hiyo itakuwa ya kuvutia haswa kutokana na jinsi timu zilivyojiandaa. Mataifa 16 yanatarajiwa kuchuana katika michuano hiyo huku viwanja vitakavyotumika vikiwa vinne ambavyo ni Bata, Malabo, Mongomo na EbebiyĆn.

No comments:
Post a Comment