Tuesday, January 27, 2015

MADRID YADAI HAIKUVUNJA SHERIA KATIKA KUSAJILI WACHEZAJI WALIO CHINI UMRI.

KLABU ya Real Madrid imetoa taarifa jana ya kudai kuwa walifuata taratibu zote za kisheria zilizowekwa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA katika usajili wa wachezaji walio chini umri wa miaka 18. Kauli hiyo imekuja kufuatia FIFA kudai kufanya uchunguzi kuhusiana na usajili wa wachezaji kadhaa walio chini umri waliosajiliwa na klabu hiyo. Mapema wakati wakimtambulisha Lucas Silva, mkurugenzi wa klabu hiyo Emilio Butragueno amesema wanajua kuwa FIFA ililiomba Shirikisho la Soka la Hispania taarifa zinazohusiana na uhamisho wa aina hiyo uliofanywa na Madrid katika kipindi cha miaka mitano. Mkurugenzi huyo amesema wataipa FIFA ushirikiano wowote watakaotaka katika uchunguzi wao kwani hawani wasiwasi kuhusu kuvunja sheria kuhusiana na suala hilo. Alhamisi iliyopita Madrid ilimsajili rasmi kiungo wa kimataifa wa Norway Martin Odegaard mwenye umri wa miaka 16 kutoka klabu ya Stroemgodset. Mahasimu wao Barcelona wapo katika kifungo cha kufungiwa kusajili misimu miwili baada ya FIFA kuwakuta na hatia ya kukiuka sheria katika usajili wa wachezaji walio chini umri wa miaka 18.

No comments:

Post a Comment