KOCHA wa timu ya taifa ya Ivory Coast, Herve Renard amesema timu bora ya mashindano imetolewa baada ya kikosi chake kuitandika Algeria na kutinga nusu fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika. Mshambuliaji mpya wa Manchester City Wilfried Bony aliifungia Ivory Coast mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-1 waliopata katika mchezo huo. Akihojiwa Renard amesema anafikiri wameifunga timu bora katika mashindano. Renard amesema walihitaji kujipanga vyema ili kujaribu kuifunga timu ambayo ni imara kwa kitimu na mchezaji mmoja mmoja. Renard ambaye aliingoza Zambia kushinda taji la michuano hiyo mwaka 2012, amesema wakati akiinoa Zambia, Ivory Coast ndio ilikuwa timu bora kuliko wao lakini waliifunga kwa changamoto ya mikwaju ya penati. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kisoka na umiliki wa mpira Algeria walikuwa bora kuliko wao lakini walitumia vyema mashabulizi yao kushtukiza wakiwategemea nyota wake Max Gradel, Gervinho na Bony.
No comments:
Post a Comment