Wednesday, March 25, 2015

MABINGWA WA DUNIA UJERUMANI KUVAA VITAMBAA VYEUSI KUOMBOLEZA WALIOFARIKI KATIKA AJALI YA NDEGE.

MABINGWA wa dunia timu ya taifa ya Ujerumani wanatarajiwa kuvaa vitambaa vyeusi na kusimama dakika moja kabla ya mchezo wao wa kirafiki utakaochezwa baadae dhidi ya Australia ili kutoa heshima zao kwa watu waliofariki katika ajali ya ndege kwenye Milima ya Ufaransa. Rais wa Chama cha Soka cha Ujerumani-DFB, Wolfgang Niersbach alithibitisha kuwepo kwa dakika moja ya maombolezo kabla ya mchezo huo wa kimataifa utakaofanyika Kaiserslautern. Zaidi ya nusu ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo wanaaminika kuwa raia wa Ujerumani. Niersbach amesema wanafanya hivyo ili watu waliopotelewa na ndugu zao katika ajali hiyo iliyotokea jana wajue kuwa familia ya soka iko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu. Wanafunzi 16 wa Ujerumani waliokuwa katika safari ya kishule wanahofiwa kuwa miongoni mwa abiria 144 na wafanyakazi sita waliouawa wakati ndege ya shirika la ndege la Germanwings ilipopata ajali wakati ikisafiri kwenda Duesseldorf kutokea Barcelona.

No comments:

Post a Comment