Wednesday, March 25, 2015

RATIBA CHAN KUPANGWA APRILI 5.

RATIBA ya mechi za kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani-CHAN inatarajiwa kupangwa Aprili 5 mwaka huu jijini Cairo, Misri. Timu zipatazo 42 zinatarajiwa kuwemo katika ratiba hiyo iliyogawanyishwa kwa kanda kutoka mataifa wanachama wa Shirikisho la Soka la Afrika-CAF. Kanda ya Kaskazini ambayo itajumuisha timu za Libya, Morocco na Tunisia watacheza wenyewe katika hatua ya mzunguko huku timu mbili za juu zikitarajiwa kufuzu kwa ajili ya fainali hizo. Kanda zingine zitakuwa zimegawanywa kama ifuatavyo, kanda ya magharibi A itakuwa na timu za Gambia, Guinea, Guinea Bissau, Liberia, Mali, Mauritania, Senegal, Sierra Leone ambapo washindi wawili ndio watasonga mbele. Magharibi B kutakuwa na Burkina Faso, Côte d’Ivoire, Ghana, Niger, Nigeria, Togo ambapo pia timu mbili ndio zitasonga mbele huku kanda ya kati ikijumuisha timu za Cameroon, Afrika ya Kati, Congo, Chad, DR Congo, Gabon na timu tatu ndio zitasonga mbele. Kanda ya kati-mashariki itakuwa na timu za Burundi, Djibouti, Ethiopia, Kenya, Sudan, Tanzania, Uganda ambapo timu tatu pia ndio zitasonga mbele huku kanda ya Kusini ikijumuisha timu za Angola, Botswana, Comoros, Mauritius, Lesotho, Mozambique, Namibia, Seychelles, South Africa, Swaziland, Zambia and Zimbabwe. Mechi za kufuzu zinatarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Juni 19 mpaka 21 na Agosti 28 mpaka 30 ambapo timu 15 zitakazofuzu zitaungana na wenyeji Rwanda katika fainali ya michuano hiyo itakayofanyika kuanzia Januari 16 mpaka Februari 7 mwakani.

No comments:

Post a Comment