Thursday, March 26, 2015

SARE YAMPA WASIWASI LOEW.

KOCHA wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Loew amedai kuwa kikosi chake kilishindwa kutumia mfumo wao wakati walipotoa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Australia katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliofanyika jana. Katika mchezo huo mabingwa hao wa dunia ndio waliotangulia kupata bao la kuongoza kupitia kwa Marco Reus kabla ya Australia kusawazisha na kuongeza bao kupitia kwa Mile Jedinak na James Troisi. Mshambuliaji Lukas Podolski aliyeingia akitokea benchi aliisawazishia Ujerumani bao katika dakika ya 81 ya mchezo na kupelekea timu hizo kutoshana nguvu katika mchezo huo. Akihojiwa kuhusiana na mchezo huo, Loew anadhani kikosi chake kilishindwa kuendeleza mipango na aina ya uchezaji walioanza nao katika kipindi cha kwanza. Kocha huyo amesema mwanzoni walitengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa kabisa kucheza mchezo wao katika kipindi cha pili hivyo kupelekea mchezo kuwaelemea.

No comments:

Post a Comment