MKURUGENZI wa michezo wa klabu ya Schalke, Horst Heldt amesisitiza kuwa kushindwa kwao kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hakuwezi kuathiri dhamira yao ya kutaka kumsajili kiungo wa Real Madrid Sami Khedira. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani alithibitisha mapema mwezi huu kuwa anatarajia kuondoka Santiago Bernabeu wakati mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huku Schalke ikiwa ni mojawapo ya vilabu vinavyowania kumsajili. Ingawa Schalke wapo katika hatari ya kuikosa michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao kutokana na kuwa nafasi ya tano katika msimamo wa Bundesliga hivi sasa, bado wana uhakika jambo hilo haliwezi kupoteza nafasi yao ya kumrejesha Khedira Ujerumani. Heldt amesema uamuzi wa mchezaji mwenyewe mara nyingi huwa hautegemei kama watafuzu michuano hiyo au la. Kiongozi huyo aliendelea kudai kuwa pamoja na kwamba wanajua hawako peke yao katika kinyang’anyiro hicho lakini ana uhakika bado wanaweza kupata saini yake mwishoni mwa msimu.
No comments:
Post a Comment