Tuesday, March 24, 2015

STARS YAWASILI MWANZA TAYARI KUWAKABILI MALAWI.

TIMU ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imewasili salama leo asubuhi jijini Mwanza, tayari kwa maandalizi ya mchezo wa kirafiki wa Kimataifa siku ya jumapili Machi 29, 2015 dhidi ya timu ya Taifa ya Malawi (The Flames), mechi itakayochezwa kwenye dimba la Uwanja wa CCM Kirumba. Kikosi cha Stars kimeondoka kikiwa na wachezaji 18 ambao wameripoti kambini jana, huku kiugo mshambuliaji Mwinyi Kazimoto anayecheza soka la kulipwa nchini Qatar akitarajiwa kuungana na wenzake leo mchana jijini Mwanza. Wachezaji waliopo kambini jijini Mwanza ni, magolikipa Aishi Manula na Mwadini Ali (Azam FC), walinzi ni Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Aggrey Morris (Azam FC) , Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Haji Mwinyi (KMKM), Hassan Isihaka na Abdi Banda (Simba SC). Wengine ni Amri Kiemba, Frank Domayo, Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla (Simba SC), Haroun Chanongo (Stand United), John Bocco (Azam FC), Juma Luizio (Zesco United), Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe). Mchezaji Mcha Khamis wa Azam FC amejiondoa kikosini kutokana na kuwa majeruhi, huku wachezaji wa Young Africans wakitarajiwa kujiunga na kikosi hicho cha timu ya Taifa mara tu baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya JKT Ruvu siku ya jumatano.

No comments:

Post a Comment