Monday, March 30, 2015

TENGA AISHUKURU TFF KWA KUMUUNGA MKONO.

MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati-CECAFA, Leodegar Chilla Tenga amelishukuru Shirikisho la Soka Tanzania-TFF kwa kumuunga mkono katika kugombea tena nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika-CAF katika uchaguzi utakaofanyika Aprili 7, mwaka huu mjini Cairo, Misri. Tenga amesema hayo katika mkutano wa pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi kuzungumzia uchaguzi wa CAF na FIFA. Tenga ni mgombea pekee wa nafasi hiyo kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati. Wakati huohuo Tenga amezungumzia pia msimamo wa bara la Afrika uliowekwa katika Mkutano Mkuu wa CAF uliofanyika mwaka jana jijini Sao Paulo, Brazil kuwa wanachama wote wa CAF watamuunga mkono Rais wa sasa wa FIFA anayetetea nafasi yake katika uchaguzi utakaofanyika Mei mwaka huu jijini Zurich, Uswisi. Vilevile Mkutano Mkuu wa CECAFA uliofanyika Desemba 2014 jijini Nairobi, Kenya ulipitisha azimio la kumuunga mkono Joseph Sepp Blatter katika uchaguzi wa FIFA. Katika mkutano huo, Rais wa TFF, Jamal Malinzi ametoa tamko rasmi kuwa kwa niaba ya TFF atampigia kura Joseph Sepp Blatter.

No comments:

Post a Comment