Tuesday, April 7, 2015

BOLT ATAMBA KUTETEA UBINGWA WAKE WA DUNIA.

MWANARIADHA nyota wa mbio za fupi na bingwa mara tatu wa michuano ya olimpiki, Usain Bolt amepiga hatua kubwa kuhakikisha anatetea ubingwa wake wa dunia msimu huu na hana wasiwasi na changamoto atakayopata kutoka kwa Justin Gatlin. Gatlin raia wa Marekani ndio aliyetawala mbio za Diamond League mwaka jana akitumia muda wa sekunde 9.77 katika mbio za mita 100 na sekunde 19.68 katika mbio za mita 200. Kocha anayemnoa Bolt, Glen Mills amesema nyota huyo wa Jamaica amepiga hatua kubwa katika maandalizi yake toka atumie muda wa sekunde 46.37 katika mbio za mita 400 zilizofanyika jijini Kingston, Jamaica Machi mwaka huu. Mills amesema Bolt amekuwa akifanya jitihada kubwa mazoezini na kama akiweza kufikia ubora wake hadhani kama kuna mwanariadha yeyote anayeweza kumtisha. Bolt mwenye umri wa miaka 28 ambaye alikimbia katika mashindano matatu pekee mwaka jana, anatarajiwa kutetea ubingwa wake wa dunia kwa mara ya tatu katika mbio za mita 100 na nne katika mbio za mita 200 katika mashindano yatakayofanyika jijini Beijing, China Agosti mwaka huu.

No comments:

Post a Comment