KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson amedokeza kuwa Jack Wilshere anaweza kukosa nafasi katika kikosi cha timu hiyo katika michuano ya Ulaya mwaka 2016. Michael Carrick ameonyesha umahiri mkubwa katika michezo miwili iliyopita dhidi ya Lithuania na Italia wakati Hodgson akiwasifu Ross Barkley na Andros Townsend kufuatia sare ya bao 1-1 waliyopata jijini Turin. Kwasasa Wilshere yuko nje ya uwanja akijiuguzi majeruhi na anakaribia kurejea tena uwanjani huku wachezaji waliopangwa kuchukua nafasi yake wakati hayupo wakionekana kuimudu vyema. Hodgson amesema vyombo vya habari vimekuwa vikimsifu Wilshere kuwa mchezaji bora katika mechi zao lakini yeye amekuwa akimhusudu zaidi Carrick na anafurahi kumuona amerejea katika ubora wake. Hata hivyo, kocha huyo aliendelea kudai kuwa bado muda uko mwingi wa kuteua kikosi chake cha mwisho kwa ajili ya michuano hiyo iitakayofanyika nchini Ufaransa.

No comments:
Post a Comment