Sunday, May 3, 2015

VIPIGO VYAIWEKA MASHAKANI UNITED.

KLABU ya Manchester United imepata kipigo cha tatu mfululizo wakati West Bromwich wakikaribia kujinasua katika hatari ya kushuka daraja. Katika mchezo huo United walimiliki vyema mchezo lakini walijikuta wakifungwa bao katika kipindi cha pili wakati mpira wa adhabu uliopigwa na Chris Brunt ulipombabatiza mchezaji mwenzake Jonas Olsson na kutinga wavuni. Hata hivyo United walipata nafasi ya kusawazisha bao hilo baada ya kupata penati kufuatia Saido Berahino kuunawa mpira katika eneo la hatari lakini penati hiyo iliyopigwa na Robin van Persie iliokolewa na golikipa wa West Brom Boaz Myhill. Kipigo hicho kinaifanya United kuendelea kubakia nafasi ya nne wakiwa alama nne juu ya Liverpool wanaoshika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo meneja wa United Louis van Gaal alilalamikia wapinzani wao kujilinda zaidi hivyo kuwapa wakati mgumu kupenya katika ngome yao.

No comments:

Post a Comment