MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger anapanga kumaliza imara msimu wa Ligi Kuu ili kuongeza morali wa kushindania taji la ligi hiyo msimu ujao. Arsenal inatarajiwa kusafiri kuifuata Hull City kesho wakiwa na matumaini ya kushinda ili kujiimarisha katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi nyuma ya bingwa mteule Chelsea. Sare ya bila ya kufungana dhidi ya Chelsea katika Uwanja wa Emirates wiki iliyopita ilififisha matumaini ya Arsenal kuwafikia vinara hao wa ligi. Akihojiwa kuelekea katika mchezo huo Wenger amesema malengo yao ni kumaliza msimu vyema na kuondoka na nguvu hiyo kwa ajili ya msimu ujao. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa Manchester City ambao kwasasa wanashika nafasi ya pili walianza imara kuliko wao hivyo kwa kipindi kirefu walikuwa mbele yao ila Manchester United hawakuwa na tofauti nao kwani wote walianza taratibu na kuimarika nusu ya pili ya msimu. Wenger amesema kikubwa kilichochangia kuanza taratibu ni michuano ya Kombe la Dunia ambapo ilibidi kuwapumzisha baadhi ya wachezaji wakati msimu umeanza huku pia wakikabiliwa na mechi za awali za kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa.
No comments:
Post a Comment