Tuesday, June 30, 2015

FAINALI YA LIGI YA MABINGWA ULAYA 2017 KUCHEZWA UWANJA WA MILLENNIUM, CARDIFF.

SHIRIKISHO la Soka la Ulaya-UEFA limethibitisha kuwa Uwanja wa Millennium uliopo jijini Cardiff ndio utakuwa mwenyeji wa mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2017. Mara ya mwisho Cardiff kuandaa mechi ya UEFA ilikuwa ni mwaka jana wakati Real Madrid walipoitandika Sevilla kwa mabao 2-0 katika mchezo wa Super Cup ambao hukutanisha bingwa Ligi ya Mabingwa na Europa League. Taarifa hizo zimeonyeha kufurahisha wachezaji nyota wa kimataifa wa Wales Gareth Bale na Aaron Ramsey ambao hawakusita kusifia hatua hiyo. Akihojiwa Bale amesema hilo ni jambo muhimu kwa soka la Wales kwani inaonekana nchi nzima iko nyuma yao wakati wakijaribu kufuzu fainali za michuano ya Ulaya zitakazochezwa mwakani nchini Ufaransa. Naye Ramsey mwenye umri wa miaka 24 alisifia hatua hiyo akidai ni muhimu kwa maendeleo ya soka la nchi hiyo. UEFA pia ilitangaza Uwanja wa Friends Arena uliopo jijini Solna, Sweden kuwa ndio utakaochezwa fainali ya michuano ya Europa League mwaka huohuo huku Uwanja wa Taifa wa Filip II uliopo huko Skopje, Macedonia wenyewe ukitumika kwa ajili ya mchezo wa Super Cup.

No comments:

Post a Comment