Friday, June 26, 2015

MECHI ZA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO KUANZA KUTIMUA VUMBI LEO.

MICHUANO ya Kombe la Shirikisho ya Afrika hatua ya makundi inatarajiwa kuanza kutimua vumbi leo kwa mchezo mmoja wa kundi A. Katika mchezo huo klabu kongwe ya Tunisia Etoile du Sahel wanatarajiwa kuikaribisha timu ya Stade Malien ya Mali katika uwanja wao nyumbani wa Seydou Tiama. Mchezo mwingine wa kundi hilo unatarajiwa kuchezwa Jumapili hii ambapo mabingwa watetezi wa kombe hilo Al Ahly ya Misri itavaana na mahasimu wao wa siku nyingi Esperance ya Tunisia katika Uwanja wa Suez Army. Katika michezo ya kundi B ambayo itachezwa kesho AC Leopards ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC wataikaribisha Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika uwanja wao wa Denis Sassou Nguesso uliopo huko Dolisie. Mchezo mwingine wa kundi hilo klabu kongwe ya Zamalek ya Misri watawakaribisha mabingwa mara tatu wa michuano hiyo CS Sfaxien ya Tunisia katika mchezo utakaofanyika katika Uwanjwa wa Michezo Petro jijini Cairo.

No comments:

Post a Comment