RAIA mmoja wa Argentina aliyetekwa nchini Nigeria, amedai kuwa jina la mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi ndio lililookoa maisha yake. Santiago Lopez Menendez mwenye umri wa miaka 28 ambaye kitaaluma ni injinia wa kilimo, alikuwa akifanya kazi Nigeria toka mwaka jana akisaidia upandaji wa mazao ya soya na nafaka katika mji wa Kontagora. Lakini mapema wiki iliyopita alitekwa na kupigwa na watu wasiojulikana ambao walikuwa hawawezi hata kuzungumza lugha ya kiingereza na kudhani alikuwa raia wa Marekani. Katika hekaheka za kujaribu kuwafafanulia kuwa yeye sio raia wa Marekani, alifanikiwa kuwatuliza watekaji wake kwa kulitaja jina la Messi mara kadhaa huku akilia. Watekaji hao walimshikilia kwa siku tatu kabla ya kumuachia baada ya kampuni ambayo ilimuajiri kuwalipa kiasi cha fedha ambacho hakikuwekwa wazi. Mara baada ya kuachiwa Menendez amesema anamshukuru Messi kwani kitendo cha kutaja jina lake ndio kilichookoa maisha yake mikononi mwa watekaji hao.
No comments:
Post a Comment