KOCHA wa timu ya taifa ya Chile, Jorge Sampaoli amedai kuwa Alexis Sanchez anahitaji kucheza kwa ubora wake wakati wakijaribu kukata kiu ya karibu karne moja kunyakuwa taji la kwanza la michuano ya Copa America. Chile walifanikiwa kutinga hatua ya fainali jana baada ya kuichapa Peru kwa mabao 2-1 na sasa wanasubiri mshindi katika mchezo wa leo kati ya Argentina wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo na Paraguay. Akihojiwa Sampaoli amesema Sanchez ni mchezaji muhimu katika kikosi chao ndio maana wanafanya kila wanaloweza kujaribu kumrejesha katika kiwango chake kabla ya mchezo wa fainali. Kocha huyo amedai kikosi chake kiko katika shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki wao kutokana na kuwa wenyeji hivyo ni muhimu kwa kila mchezaji kuwa fiti kwa asilimia 100 katika mchezo huo. Fainali ya michuano hiyo ambayo ilianzishwa miaka 99 iliyopita inatarajiwa kupigwa katika Uwanja wa Taifa uliopo jijini Santiago Jumamosi hii.
No comments:
Post a Comment