FAINALI ya michuano ya Copa America inatarajiwa kupigwa kesho huku Argentina wanaopewa nafasi kubwa ya kunyakuwa taji hilo wakiwa na kibarua kizito mbele wenyeji wa michuano hiyo Chile. Argentina wakiongozwa na Lionel messi watajitupa katika Uwanja wa Taifa uliopo jijini Santiago wakiwa na ndoto za kukata kiu ya mataji iliyolikumba taifa hilo kwa kipindi cha miaka 22. Mara ya mwisho Argentina kunyakuwa taji ilikuwa ni mwaka 1993 na miezi 12 iliyopita walikaribia kufanya hivyo walipotinga fainali ya Kombe la Dunia lakini bahati haikuwa yao kwani walifungwa na Ujerumani. Kwa upande wa Chile wao wanataka kutumia nafasi hiyo ya kipekee kunyakuwa taji lao la kwanza la michuano hiyo na kuondoa machungu ya miaka 99 ya kutoka kapa. Baada ya kusuasua katika hatua ya makundi huku wakija kuifunga Colombia kwa changamoto ya mikwaju ya penati katika robo fainali, Argentina wanaonekana kuimarika katika kiwango chao kwa wakati muafaka baada ya kuitandika Paraguay kwa mabao 6-1 katika mchezo wa nusu fainali. Chile wakiwa na nyota wao Alexis Sanchez, Arturo Vidal na Claudio Bravo wataingia katika mchezo wa kesho huku wakiwa na kumbukumbu mbaya kwani katika mechi 24 walizowahi kukutana katika michuano hiyo na Argentina hawajawahi kupata ushindi hata moja.
No comments:
Post a Comment