WANDAAJI wa michuano ya Kombe la Dunia la wanawake, wamedai kuwa wachezaji huwa hawajali mtu anayewakabidhi zawadi na kutokuwepo kwa rais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Sepp Blatter hakuathiri fainali ya michuano hiyo. Kutokana na uchunguzi wa masuala ya ufisadi unaondelea katika shirikisho hilo, wakili wa Blatter alikaririwa akidai kuwa mteja wake huyo hatasafiri kwenda jijini Vancouver, Canada kushuhudia mchezo wa fainali kati ya Marekani na Japan kesho. Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Blatter kutokabidhi zawadi kwa mshindi wa michuano hiyo ya wanawake ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne, toka achaguliwe kuliongoza shirikisho hilo mwaka 1998. Akihojiwa kuhusiana na hilo rais wa Chama cha Soka cha Canada, Victor Montagliani amesema kiukweli wachezaji huwa hawajali sana mtu anayewapa zawadi hivyo kukosekana kwa Blatter hadhani kama kutakuwa na tatio lolote.
No comments:
Post a Comment