BEKI wa kimataifa wa Uingereza Lucy Bronze ametajwa katika orodha ya tuzo za Mpira wa Dhahabu, tuzo ambayo atapewa mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Dunia la wanawake. Bronze mwenye umri wa miaka 23 alifunga bao maridadi wakati Uingereza ilipoichapa Norway katika hatua mtoano huku pia akifunga katika mchezo wa robo fainali dhidi ya wenyeji Canada. Hata hivyo Uingereza waliondolewa katika hatua ya nusu fainali kwa kutandikwa na Japan mabao 2-1. Mfungaji bora wa michuano hiyo mpaka sasa Celia Sasic wa Ujerumani ambaye ana mabao sita na pia ni miongoni mwa wachezaji nane waliotajwa katika orodha hiyo. Kiungo wa China Jiali Tang, mshambuliaji wa Norway Ada Hegerberg na beki wa Canada Kadeisha Buchanan wote hao wametajwa katika orodha ya tuzo za wachezaji chipukizi. Kwa upande wa orodha ya tuzo kipa bora wa mashindano wapo Nadine Angerer wa Ujerumani, Ayumi Kaihori wa Japan na Hope Solo wa Marekani. Washindi watachaguliwa na kamati ya ufundi wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA na kutangazwa mara baada ya mchezo wa fainali Jumapili hii utakaowakutanisha Marekani na bingwa mtetezi Japan.
No comments:
Post a Comment