MECHI za kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2017, zilirindima wikiendi iliyopita huku tukishuhudia viwanja mbalimbali kutoka pembe zote za bara la Afrika vikiwaka moto. Katika mechi za jana, mabingwa wa zamani wa Afrika Misri waliichapa bila huruma Chad kwa mabao 5-0 huku mabingwa watetezi Ivory Coast ambao walimkosa nyota wao Yaya Toure waking’ang’aniwa sare ya bila kufungana na Sierra Leone. Cameroon wao walipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Gabon na Afrika ya Kati waliishangaza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC kwa kuitandika mabao 2-0. Libya walishindwa kuzitumia vyema penati mbili walizopata na kujikuta wakichapwa mabao 2-1 na Cape Verde huku Benin wao wakitoka sare ya bao 1-1 na mali. Misri sasa ndio wanaongoza kundi G wakiwa na alama sita, wakifuatiwa na Nigeria waliopo nafasi ya pili kwa kuwa na alama nne baada ya kutoka sare tasa na Tanzania wanaoshika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama moja na Chad inaburuza mkia wakiwa hawana alama yeyote. Kwa upande wa kundi I ambalo lina timu tatu Sudan ndio wanaoongoza wakiwa na alama tatu wakifuatiwa na Ivory Coast na Sierra Leone wenye alama moja kila mmoja. Cameroon wao ndio vinara wa kundi M wakifuatiwa na Mauritania wenye alama tatu na Gambia na Afrika Kusini ndio wanaofuata kwa kuwa na alama moja kila mmoja. Kundi B linatawaliwa na Angola wenye alama nne, wakifuatiwa na Afrika ya Kati na DRC wenye alama tatu kila mmoja na Madagascar wanaburuza mkia kwa kuwa na alama moja. Mali ni wababe wa kundi C wakiwa na alama nne wakifuatiwa na Sudan Kusini wenye alama tatu, Benin wako nafasi ya tatu kwa kuwa na alama mbili na Equatorial Guinea wanaburuza mkia wakiwa na alama moja. Mechi za mzunguko wa tatu zinatarajiwa kuchezwa tena Machi mwakani.
No comments:
Post a Comment