Wednesday, November 25, 2015

CHAMPIONS LEAGUE ROUND UP.

MABINGWA watetezi wa michuano ya Ligi ya Mabingwa, Barcelona jana wamefanikiwa kufuzu hatua ya timu 16 bora kufuatia ushindi mnono waliopata dhidi ya AS Roma ya Italia. Katika mchezo huo Barcelona wakiwa katika ubora wao waliwachakaza waitaliano hao kwa mabao 6-1 ambayo yalifungwa kwa ustadi mkubwa na Luis Suarez na Lionel Messi waliofunga mawili kila mmoja pamoja na Gerard Pique na Adriano. Barcelona waligundua mapema kuwa wamefuzu hatua ya mtoano kabla ya kuanza kwa mchezo huo uliofanyika Camp Nou kufuatia BATE Borisov kutoka sare ya bao 1-1 na Bayer Liverkusen ya Ujerumani katika mchezo uliofanyika mapema huko Belarus. Wengine waliofanikiwa kufuzu jana ni mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich ambao bila ya huruma waliichakaza Olympiakos kwa mabao 4-0 katika mchezo uliofanyika Allianz Arena na kutoa mwanya kwa Arsenal walioshinda mchezo wao dhidi ya Dinamo Zagreb kwa mabao 3-0 kufufua upya matumaini yao ya kufuzu. Kama Bayern na Olympiakos wangetoka sare katika mchezo huo wote wawili wangefuzu hatua inayofuatia hivyo kuwaacha Arsenal wakiangukia katika michuano ya Europa League. Nao mabingwa Ligi Kuu Chelsea walikwea kileleni mwa kundi G kwa kuwachapa vibonde Maccabi Tel Aviv ya Israel kwa mabao 4-0 huku mchezo mwingine wa kundi hilo ukishuhudia Dynamo Kiev ya Ukraine wakiicharanga FC Porto ya Ureno kwa mabao 2-0.

No comments:

Post a Comment