POLISI nchini Ujerumani wamevamia ofisi za Shirikisho la Soka la Ujerumani-DFB na nyumbani kwa rais wake Wolfsgang Niersbach kufuatia madai ya rushwa yanahusiana na kupata kwao haki ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2006. Kashfa ya ufisadi iliyolikumba Shirikisho la Soka Duniani-FIFA imehusisha pia madai kuhusu utolewaji zabuni iliyowapa Ujerumani uenyeji wa Kombe la Dunia 2006, huku kamati ya maadili ya FIFA mwezi uliopita ikianzisha uchunguzi dhidi ya nguli wa zamani wa Ujerumani Franz Beckerbauer ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya maandalizi. Nguli huyo wa zamani wa Bayern Munich amekiri kuwa malipo yalifanyika kwenda FIFA wakati mchakato wa kutafuta uenyeji ukiendelea lakini akasisitiza ilikuwa sehemu ya kurudisha baadhi ya gharama. Habari hiyo imechukua uelekeo mwingine leo kufuatia wachgunguzi kuanza kusachi ofisi za makao makuu ya DFB zilizoko huko Frankfurt pamoja na nyumbani kwa rais Niersbach. Waendesha mashitaka wa Frankfurt wameanzisha uchunguzi huo wakihisi kuna kodi ilikwepwa kulipwa kipindi hicho cha utoaji zabuni hiyo na fedha kiasi cha euro milioni 6.7 za kamati ya maandalizi zilizotolewa na DFb kwenda FIFA.
No comments:
Post a Comment