Friday, December 4, 2015

HAYATOU ASINZIA KATIKA MKUTANO NA WANAHABARI.

RAIS wa Shirikisho la Soka la Afrika-CAF ambaye kwasasa ana kaimu nafasi ya urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Issa Hayatou jana usiku aliwashangaza wanahabari baada ya kusinzia akiwa katika mkutano. Inafahamika kwamba kumekuwa na pilikapilika nyingi ndani ya shirikisho hilo baada ya maofisa kadhaa kukamatwa jijini Zurich lakini ni jambo ambalo halikutegemewa kwa Hayatou kuchagua muda huo kusinzia ambao dunia nzima ilikuwa ikimuangazia. Hayatou amekaimu madaraka hayo baada ya rais Sepp Blatter kusimamishwa kwa siku 90 kupisha uchunguzi wa tuhuma za ufisadi ambazo zinamkabili pia makamu wake Michel Platini. Mapema katika mkutano huo Hayatou alikanusha minong’ono iliyokuwa ikijitokeza kuwa na yeye anahusika kwa namna moja au nyingine katika kashfa za rushwa ambazo zimekuwa zikilizonga shirikisho hilo. Hayatou amesema kama angekuwa anahusika hadhani kama angekuwa katika nafasi hiyo hivi sasa na kuongeza kuwa atajitahidi kufanya kila wawezalo kuhakikisha wanarejesha jina zuri la FIFA mpaka ifikapo kipindi cha uchaguzi wa rais mpya Februari mwakani.

No comments:

Post a Comment