BEKI wa zamani wa Barcelona, Carles Puyol anaamini itakuwa ni ukosefu wa haki kama Lionel Messi asiposhinda tuzo ya Ballon d’Or kwa mara ya tano baadae leo. Macho na masikio ya wapenzi wa soka duniani kote leo yataelekezwa jijini Zurich, Uswisi ambako kutafanyika sherehe hizo za kumtafuta mfalme wa soka duniani. Pamoja na kuwepo tuzo nyingi katika sherehe hizo lakini kinachosubiriwa kwa hamu ni ile ambayo itawapambanisha nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo ambaye atachuana sambamba na nyota wa Barcelona Lionel Messi na Neymar. Messi ndio anayepewa nafasi kubwa ya kutwa tuzo hiyo kutoka hasimu wake Ronaldo ambaye alishinda tuzo yake ya tatu ta Ballon d’Or msimu uliopita. Akihojiwa Puyol ambaye amecheza na Messi mwenye umri wa miaka 28 kwa misimu 10, amesema huwezi kujua kitakachotokea lakini anadhani itashangaza kama nyota huyo asiposhinda tuzo hiyo. Mwaka jana ulikuwa mzuri kwa Messi kwani aliiwezesha timu yake kushinda mataji matano yakiwemo lile la La Liga, Kombe la Mfalme, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Super Cup ya Hispania na Klabu Bingwa ya Dunia huku akifunga mabao 48 katika kipindi mwaka mzima mwaka jana.
No comments:
Post a Comment