Friday, January 15, 2016

WATFORD WACHUKUA TUZO MBILI ZA MWEZI.

KLABU ya Watford imefanikiwa kupata tuzo mbili baada ya mshambuliaji Odion Ighalo kupata tuzo ya mchezaji bora wa mwezi na meneja wake Quique Sanchez Flores naye kupata tuzo ya kocha bora wa mwezi Desemba mwaka jana. Watford ambao wanashikilia nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu, mwezi uliopita walifungwa mara moja na Tottenham Hotspurs katika mechi tano, wakizifunga Norwich City mabao 2-0 na Liverpool mabao 3-0 katika mechi walizocheza nyumbani. Huku zile za ugenini wakishinda bao 1-0 dhidi ya Sunderland na kutoa sare ya mabao 2-2 dhidi ya mabingwa Chelsea katika Uwanja wa Stamford Bridge. Ighalo amefunga mabao matano mwezi uliopita yakiwemo mawili katika mchezo dhidi ya Liverpool na moja katika mechi dhidi ya Norwich, Sunderland na Spurs. Nyota huyo wa kimataifa wa Nigeria ambaye amefikisha mabao 14 msimu huu, atataka kuongeza idadi hiyo wakati watakaposafiri kuifuata Swansea City Jumatatu ijayo.

No comments:

Post a Comment