MSHAMBULIAJI nyota wa Leicester City, Jamie Vardy ameapa kuendelea kubakia katika klabu hiyo baada ya kufunga bao matata katika ushindi wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya Liverpool jana. Vardy aliipatia bao la kuongoza timu yake katika dakika ya 60 ya mchezo kabla ya kuongeza lingine dakika 11 baadae na kuwapa ushindi huo muhimu ambao umewafanya kuendelea kuongoza Ligi Kuu. Vardy sasa anakuwa amefikisha mabao 18 ya ligi aliyofunga na kumfanya kuzidiwa bao moja na nyota wa Real Madrid Cristiao Ronaldo na Luis Suarez wa Barcelona ambao kila mmoja amefunga mabao 19 katika La Liga msimu huu. Vardy ambaye miaka michache iliyopita alikuwa akicheza katika ligi za chini, yuko katika mazungumzo ya mkataba mpya na klabu yake hiyo ambao utamuwezesha kupata nyongeza ya mshahara kufikia paundi 80,000 kwa wiki. Akihojiwa Vardy amesema hakuna kitu kinachosemwa na watu ambacho hakijui lakini ukweli ni kuwa anapenda kuendelea kuitumikia Leicester kwa kipindi kirefu kijacho.
No comments:
Post a Comment