MENEJA wa zamani wa Uingereza, Sven Goran Eriksson anaamini fedha zinazotolewa katika soka la China ni nzuri kiasi ambacho ni vigumu kwa wachezaji wenye majina makubwa kukataa. Nyota kadhaa akiwemo Ramires, Jackson Martinez na Alex Teixeira wote wamekimbilia China na Eriksson ambaye anafundisha klabu ya Shanghai SIPG anaamini wapo wengi watakaokuja kutokana na mishahara minono wanayolipwa. Akihojiwa Eriksson amesema huwezi kuondoa ukweli kuwa fedha ndio kivutio kikubwa kwa nyota kadhaa kukimbilia nchini China. Eriksson aliendelea kudai kuwa michuano ya Ligi ya Mabingwa ya Asia ilikuwa ikitawaliwa na timu kutoka Japan, Korea Kusini na Australia lakini Guangzhou Evergrande ambayo inafundishwa na Luiz Felipe Scolari wameshinda taji hilo mara mbili katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa soka la China kwasasa linakuwa kwa kasi ndio maana inavutia wachezaji wengi wenye majina makubwa hivyo hana shaka wako wengi watakaofuatia.
No comments:
Post a Comment