Wednesday, April 6, 2016

HART FITI KUIVAA PSG.

MENEJA wa Manchester City, Manuel Pellegrini amekiri kuwa Joe Hart yuko fiti kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain utakaochezwa baadae leo. Hart alitolewa nje kwa machela baada ya kuumia katika mchezo dhidi ya Manchester United Machi 20 mwaka huu lakini alianza mazoezi jana kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa huko Parc des Princes. Akizungumza na wanahabari, Pellegrini amesema Hart alifanya mazoezi bila kuonyesha tatizo lolote na kuna uwezekano wa kumtumia kutokana na kuruhusiwa na madaktari. Kurejea kwa kipa huyo namba moja kunatoa ahueni kwa City ambao pia kiungo wao Fabian Delph aliyekuwa nje ya uwanja toka Februari naye amerejea mazoezini jana. Hata hivyo, kiungo Yaya Toure aliyeumia kisigino katika mchezo dhidi ya United, nahodha Vincent Kompany na Raheem Sterling wanatarajiwa kukaa nje katika mchezo huo.

No comments:

Post a Comment