NYARAKA zilizovuja kutoka katika mtandao wa Football Leaks, zimebainisha kuwa James Rodriguez anaweza kuigharimu Real Madrid zaidi ya euro milioni 90. Nyota huyo wa kimataifa wa Colombia, alitua Madrid akitokea Monaco mwaka 2014 kwa ada ya euro milioni 75, lakini dili hilo lilijumuisha malipo mengine ya ziada ambayo yanaweza kuifanya klabu hiyo ya Ligue1 kupata euro milioni 15 zaidi. Katika makubaliano yao Madrid wanatakiwa kuipa euro milioni moja Monaco kila wakati wanafuzu hatua inayofuata katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kuanzia msimu wa 2014-2015, makubaliano ambalo yatakuwa kwa kipindi cha miaka sita. Kiasi kingine kitakachotakiwa kulipwa na Madrid ni euro milioni tano kama Rodriguez atateuliwa katika orodha ya tuzo za Ballon d’Or katika kipindi chochote cha muda huo na kitalipwa mara moja pekee. Madrid watatakiwa kulipa kiasi kingine cha euro milioni tano kwa Monaco kama nyota huyo atashinda tuzo hiyo makubaliano ambayo yapo mpaka msimu wa 2019-2020. Kama fedha zote hizo zikilipwa kwa mujibu wa makubaliano Madrid watakuwa wamemnunua mchezaji huyo kwa kiasi cha euro milioni 90, hivyo kumfanya kuwa mchezaji wa tatu ghali duniani nyuma ya wachezaji wenzake Cristiano Ronaldo na Gareth Bale.

No comments:
Post a Comment