KIPA wa Leicester City, Kasper Schmeichel kwa kipindi kirefu amekuwa akifananishwa na baba yake Peter na sasa anaweza kuongeza kufanana kwao katika orodha baada ya kushinda taji la Ligi Kuu juzi usiku. Katika hali ya kushangaza wawili hao wameshinda mataji yao ya kwanza wakiwa na umri wa miaka 29 katika siku hiyohiyo ya Jumatatu lakini wakipishana miaka 23 na pia wote wameshinda taji hilo bila kukanyaga uwanjani. Leicester walitwaa taji hilo kufuatia sare ya mabao 2-2 waliyopata Tottenham Hotspurs dhidi ya Chelsea katika Uwanja wa Stamford Bridge, ambapo wachezaji wengi wa timu hiyo wlaiutizama mchezo huo wakiwa nyumbani kwa mwenzao Jamie Vardy.
Mwaka 1993 Peter Schmeichel akiwa na Manchester United walitwaa taji lao la kwanza la Ligi Kuu wakiwa chini ya Sir Alex Ferguson muda mchache kabla ya hawajaingia uwanjani kufuatia wapinzani wao karibu wakati huo Aston Villa kukubali kipigo kutoka kwa Oldham. Pia wawili hao wametengeneza historia nyingine ya kuwa familia ya pili ya baba na mtoto kutwaa taji hilo baada ya mshambuliaji wa Arsenal Ian Wright kufanya hivyo mwaka 1998 na kijana wake winga wa zamani wa Chelsea Shaun Wright-Philips kufanya hivyo mwaka 2006. Leicester pia wameweka historia ya kuwa bingwa wa kwanza mpya katika Ligi Kuu katika kipindi cha miaka 38 baada ya Nottingham Forest kutwaa taji hilo mwaka 1978.
No comments:
Post a Comment