Thursday, May 12, 2016

REAL MADRID YAENDELEA KUONGOZA ORODHA YA VILABU TAJIRI.

KLABU sita za Ligi Kuu Uingereza zimechomoza katika orodha ya klabu 10 zenye thamani zaidi duniani kwa mwaka huu zinazotolewa na jarida la Forbes lakini Real Madrid bado wameendelea kung’ang’ania kileleni. Klabu hiyo ya Hispania bado imeendelea kutamba katika orodha hiyo ikiwa na thamani inayokadiriwa kufikia paundi bilioni 2.515 wakiwazidi mahasimu wao Barcelona ambao wako nafasi ya pili kwa thamani ya paundi bilioni 2.449. Hata hivyo, kukua kifedha kwa ligi ya Uingereza kumepelekea klabu sita zinazoshiriki Ligi Kuu kuingia katika kumi bora na kufanya kuwa na idadi ya jumla ya timu nane katika orodha ya 20 bora. Manchester United ndio wanaongoza kwa timu hizo za Uingereza na wa tatu kwa ujumla wakiwa na thamani ya paundi milioni 2.289, wakifuatiwa na Arsenal, Manchester City, Chelsea na Liverpool katika nafasi ya tano mpaka ya nane huku Tottenham Hotspurs nao wakikwea mpaka nafasi ya 10. Bayern Munich ya Ujerumani wako nafasi ya nne na Juventus nafasi ya tisa hivyo kukamilisha orodha ya timu 10 bora zenye thamani zaidi kwasasa. Timu zingine za Uingereza zilizopo katika nafasi 20 bora ni West Ham United waliopo nafasi ya 17 na Newcastle United ambao wameteremka daraja msimu huu wakiwa nafasi ya 20.

No comments:

Post a Comment