KIUNGO wa Olympique Lyon, Mathieu Valbuena amedai kusikitishwa baada ya kuachwa katika kikosi cha wachezaji 23 wa timu ya taifa ya Ufaransa ambacho kitashiriki michuano ya Euro 2016. Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps alichagua kutomchukua kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31 ambaye ameitumikia nchi hiyo mechi 50 toka aitwe kwa mara ya kwanza mwaka 2010, huku akisisitiza uamuzi wake unatokana na nyota huyo kutokuwa fiti. Valbuena amekuwa akisumbuliwa na majeruhi mara kwa mara msimu huu hatua mabayo imemfanya kucheza mechi chache katika klabu yake. Hata hivyo, Valbuena pia anadaiwa kuachwa kutokana na sakata lake linaloendelea nje ya uwanja msimu huu likimhusisha mchezaji mwenzake Karim Benzema ambaye naye ametemwa katika kikosi hicho. Kiungo huyo alituma ujumbe akielezea kusikitishwa kwake kuachwa katika kikosi hicho lakini aliongeza ataendelea kuiunga mkono nchi yake katika michuano hiyo itakayofanyika katika ardhi ya nyumbani kwao.
No comments:
Post a Comment