Wednesday, June 8, 2016

OBAMA KUTOHUDHURIA MAZISHI YA MOHAMMAD ALI.

RAIS wa Marekani, Barack Obama anatarajiwa kukosa mazishi ya bondia nguli Muhammad Ali Ijumaa hii kwasababu ya kuingiliana na sherehe za maafali ya binti yake. Viongozi kadhaa kutoka sehemu mbalimbali duniani watakuwa miongoni mwa maelfu ya waombolezaji watakaohudhuria mazishi hayo huko Louisville, Kentucky ambako Ali alizaliwa mwaka 1942. Ikulu ya Marekani imesema kuwa Obama na mkewe Michelle wanatarajiwa kuwa katika maafali ya binti yao Malia huko Washington, DC. Ali alifariki dunia Ijumaa iliyopita hospitalini huko Phoenix, Arizona akiwa na umri wa miaka 74. Familia ya Obama inatarajia kutuma barua kwa familia ya Ali ambayo itawasilishwa na mshauri mwandamizi wa Ikulu Valerie Jarrett ambaye anamfahamu Ali. Msemaji wa familia ya Ali, Bob Gunnell amesema Obama alizungumza na mjane wa Ali, Lonnie katika simu kumpa pole kwa kifo hicho cha mmewe. Miongoni mwa viongozi watakaohudhuria mazishi hayo ni pamoja na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Mfalme Abdullah wa Jordan.

No comments:

Post a Comment