MENEJA wa klabu ya Sunderland, Sam Allardyce anatarajiwa kuteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Uingereza huku uthibitisho wake ukitegemewa kutolewa wakati wowote leo. Meneja huyo anatarajiwa kuondoka Sunderland baada ya miezi tisa ya kuinoa klabu hiyo ya Ligi Kuu. Allardyce atachukua nafasi ya Roy Hodgson ambaye alijiuzulu Juni mwaka huu baada ya Uingereza kutandikwa na vibonde Iceland katika hatua ya 16 bora ya michuano ya Ulaya iliyofanyika mwaka huu. Meneja huyo mwenye umri wa miaka 61, ambaye amewahi kuzinoa timu za West Ham United, Newcastle United, Bolton Wanderers na Nottingham Forest, alizungumza na Chama cha Soka cha nchi hiyo-FA wiki iliyopita na sasa amechaguliwa badala ya meneja wa Hull City Steve Bruce. Kitu pekee kilichobakia hivi sasa ni mazungumzo ya kuilipa fidia Sunderland kwani Allardyce alikuwa amebakisha mkataba wa mwaka mmoja katika klabu hiyo.
No comments:
Post a Comment