SHIRIKISHO la Soka la Marekani limetangaza kuwa kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo kitacheza mchezo wa kwanza wa kimataifa wa kirafiki Octoba 7 mwaka huu jijini Havana, Cuba ikiwa imepita karibu miaka 70 toka wafanye hivyo. Mchezo huo ambao utakuwa mahsusi kwa ajili ya kudumisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili, utakuwa wa kwanza toka mwaka 1947 na mara ya pili pekee kwa timu ya Marekani kutembelea kisiwa hicho toka wakati huo. Mahasimu hao wa kisiasa pia walikutana jijini Havana mwaka 2008 katika mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 iliyofanyika Afrika Kusini ambapo Marekani ilishinda kwa bao 1-0. Machi mwaka huu wakati alipotembelea Havana, rais wa Marekani Barack Obama alihudhuria mchezo wa maonyesha kati ya timu ya Baseball ya Tampa Bay Rays dhidi ya timu ya taifa ya Cuba, ikiwa timu ya kwanza kubwa kutoka Marekani kwenda huko toka mwaka 1999. Luninga za Marekani zinatarajiwa kuonyesha moja kwa moja mchezo huo wa soka utakaofanyika katika Uwanja wa Pedro Marrero.
No comments:
Post a Comment