Monday, July 11, 2016

URENO YAKWEA NAFASI MBILI VIWANGO VYA FIFA PAMOJA NA KUTWAA TAJI LA EURO 2016.

MABINGWA wa Ulaya, Ureno wanatarajiwa kukwea mpaka katika nafasi ya sita katika msimamo mpya wa viwango vya ubora vinavyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Ureno walikuwa nafasi ya nane kabla ya kuanza kwa mashindano hayo na wanakwea kwa nafasi mbili pekee baada ya kushinda mechi zao tatu kati ya saba walizocheza katika michuano hiyo huku ushindi wa changamoto ya mikwaju ya penati dhidi ya Poland ukihesabiwa kama sare. Taifa hilo lilikuwa linashika nafasi ya tatu miaka miwili iliyopita, lakini sasa hivi watashika nafasi ya sita pamoja na kushinda taji lao la kwanza kubwa kwa ushindi wa bao 1-0 waliopata katika muda wa nyongeza dhidi ya Ufaransa jana. Ufaransa wao ilikuwa wakwee mpaka nafasi ya tatu katika viwango hivyo lakini kufungwa kwao katika hatua hiyo kunaifanya kutoka nafasi ya 10 mpaka ya saba hivi sasa. Argentina wao wataendelea kuwa vinara kwenye orodha hizo kufuatia kutinga katika fainali tatu katika kipindi cha miaka mitatu na Ubelgiji wataendelea kubaki nafasi ya pili baada ya kutinga robo fainali ya michuano ya Ulaya. Tano inakamilishwa na Colombia waliopo nafasi ya tatu, Ujerumani nafasi ya nne na mabingwa wa Copa America Chile wao wako anfasi ya tano.

No comments:

Post a Comment