Wednesday, August 17, 2016

BRAZIL YAPATA NAFASI YA KULIPA KISASI KWA UJERUMANI OLIMPIKI.

TIMU ya taifa ya Brazil inatarajiwa kukwaana na Ujerumani katika hatua ya fainali ya michuano ya soka ya Olimpiki kwa wanaume Jumamosi hii. Hiyo itakuwa nafasi ya kipekee kwa Brazil kulipa kisasi kufuatia kipigo kizito cha mabao 7-1 walichopata kutoka kwa Ujerumani katika nusu fainali ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 ambayo pia ilifanmyika Brazil. Brazil walifikia hatua hiyo kwa staili ya aina yake katika Uwanja wa Maracana kufuatia kuisambaratisha Honduras kwa mabao 6-0 na kuweka hai matumaini yao ya kutwaa medali yao ya kwanza ya dhahabu ya Olimpiki. Katika mchezo huo Neymar aliweka historia kwa kufunga bao la mapema zaidi katika michuano hiyo ambalo alifunga zikiwa zimepita sekunde 14 toka kuanza kwa mchezo. Kwa upande wa Ujerumani wao walitinga hatua hiyo baada ya kuibugiza Nigeria kwa mabao 2-0 ambapo wawakilishi hao wa Afrika watacheza na Honduras kwa ajili ya kugombea medali ya shaba ya mshindi wa tatu.

No comments:

Post a Comment