MSHAMBULIAJI wa AS Monaco, Radamel Falcao anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa wiki kadhaa kufuatia kupata majeruhi katika mchezo wa kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Fenerbahce. Nyota huyo wa kimataifa wa Colombia ambaye amerejea Monaco baada ya kushindwa kung’aa katika klabu za Manchester United na Chelsea, alitengeneza bao la kuongoza kabla ya kufunga bao la pili katika ushindi wa mabao 3-1 waliopata Jumanne iliyopita. Lakini alilazimika kutolewa nje wakati wa mapumziko kufuatia kuumia mguu wake wa kulia na sasa klabu hiyo imedai kuwa atakaa nje kwa wiki kadhaa akijiuguza. Monaco ililipa ada iliovunja rekodi ya klabu ya euro milioni 60 kwa ajili ya kumsajili Falcao mwaka 2013 lakini katika msimu wake wa kwanza tu aliumia goti vibaya kabla ya misimu mingine miwili kwenda kucheza kwa mkopo nchini Uingereza.

No comments:
Post a Comment