RAIS wa Argentina, Mauricio Macri amesema hana shaka kuwa Lionel Messi atarejea katika kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi. Messi alifanya uamuzi wa kushtukiza wa kustaafu soka la kimataifa kufuatia kushindwa kwa Argentina katika fainali ya michuano ya Copa America dhidi ya Chile ikiwa ni mara ya tatu mfululizo kwa timu hiyo kushindwa fainali kwenye michuano mikubwa. Kocha mpya wa Argentina, Edgardo Bauza amesema mapema wiki hii kuwa kipaumbele chake cha kwanza ni kumshawishi Messi kubadili uamuzi wake na amepanga kusafiri kwenda Ulaya ili kujaribu adhma yake hiyo. Rais huyo wa Argentina ambaye alikuwepo jijini Rio de Janeiro kwa ajili ya ufunguzi wa mashindano ya Olimpiki, amesema alizungumza na Messi na ana uhakika atarudisha moyo wake nyuma na kusahau yaliyopita.

No comments:
Post a Comment