KLABU ya Manchester City imefanikiwa kumsajili rasmi John Stones kutoka Everton kwa kitita cha paundi milioni 47.5 na kumfanya kuwa beki wa pili ghali duniani. Nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 22, ametia saini ya mkataba wa miaka sita na anakuwa mchezaji wa nane kusajiliwa na City chini Pep Guardiola kiangazi hiki. Mapema leo jina la Stones lilionekana katika orodha rasmi ya kikosi cha City ambacho kitashiriki michuano ya kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabigwa Ulaya kabla ya kuthibitishwa rasmi. City wanatarajiwa kucheza na Steaua Bucharest ya Romania katika hatua ya kufuzu makundi, mechi ambazo zitachezwa Agosti 17 na marudiano Agosti 23 mwaka huu. Beki wa kimataifa wa Brazil, David Luiz ndio beki ghali zaidi katika historia, kufuatia uhamisho wake aliofanya kutoka Chelsea kwenda Paris Saint-Germain mwaka 2014.

No comments:
Post a Comment